Saturday, August 23, 2014

MTOTO AKIWA ANALIA SANA (Excessive Crying on a Child)

Mtoto kulia ni jambo la kawaida, ni njia ambayo watoto huitumia kuwasiliana.
Watoto walio chini ya miaka miwili hutumia kulia kama lugha yao kuu kuwasilisha mahitaji yao kuliko lugha nyinginezo. Ni muhimu kwa wazazi kumuelewa mtoto wao ili waweze kujua wakati analia kawaida, na wakati analia zaidi ya kwawaida. Pia ni vyema kumjengea mtoto tabia ya kutumia lugha nyingine tofauti na kulia kadri anavyokua.

Ni mara chache sana kwa mtoto aliye chini ya miaka miwili kulia sana bila sababu, hivyo haishauriwi kupuuzia tu au kuendelea kumbembeleza bila kujua sababu inayomfanya alie; ni vyema kuchunguza kwanza sababu inayomfanya aendelee kulia.

Kwa upande mwingine wazazi wengi, hasa wale wapya, huhamaki wanapoona mtoto analia kuliko kawaida na kushindwa kujua wafanye nini kumsaidia. Ukurasa huu ukusaidie kama mzazi au mlezi wa mtoto kufahamu hatua za kuchukua unapokuwa na mtoto wakati analia sana.


SABABU ZA MTOTO KULIA SANA

- Homa ya uti wa mgongo
- Malaria kali (ya kichwa)
- Homa ya masikio
- Kuumia au kuvunjika
- Tumbo kuuma au gesi tumboni
- Michubuko au vidonda mdomoni, kooni au vitokanavyo na nepi
- Choo kigumu (constipation)
- Kuchoka sana au kushindwa kulala
- Njaa ya muda mrefu
- Kuumwa na mdudu kama siafu n.k.
- Nguo kubana au kufunikwa sana
- Kutaka kuwa na mzazi wake!
- Magonjwa ya kisaikolojia


UFANYE NINI MTOTO AKIWA ANALIA SANA:

NAMNA YA KUM'BEBA: 

- Mbebe mtoto katika hali itakayompa utulivu
o Mweke begani au kumpakata kama inavyoonekana kwenye picha.

o Hali ya utulivu humwezesha mtoto aliyechoka sana kupata usingizi.
o Kumweka begani husaidia kuondoa gesi tumboni.

NAMNA YA KUMBEMBELEZA

 - Haishauriwi kumrusha rusha mtoto au kumtingisha kwa nguvu
o Huongeza maumivu kwa mtoto aliyeumia au kuvunjika
o Humfanya mtoto mwenye homa au tatizo la tumbo kujisikia vibaya zaidi
o Humfanya mtoto aliyechoka sana kushindwa kulala na kumfanya azidi kulia.

MAMBO YA MUHIMU KUCHUNGUZA:

- Muda na mazingira alipoanza kulia:
o Hali ya mtoto kabla hajaanza kulia – aliyelala, anacheza, anakula, n.k
o Kilichotokea au kusababisha akaanza kulia – kushtuka, kuanguka, kula, ghafla tu n.k
o Mazingira aliyokuwepo alipoanza kulia – chumbani, bafuni, kwenye majani, jikoni n.k

Chakula :

o Muda aliokula mlo wa mwisho
o Chakula alichokula na kiasi alichokula.
o Mabadiliko katika chakula chake (hata kama ni madogo) – uandaaji au kumlisha
o Kwa mtoto anayenyonya mama achunguze kama kuna mabadiliko yeyote katika maziwa yake (kama maziwa hayatoki, au yanauma au chuchu zina michubuko)

Choo chake:

o Muda alipopata choo mara ya mwisho (kikubwa au kidogo)
o Muda aliobadilishwa nepi; Pia chunguza nepi aliyovaa.
o Muonekano wa choo alichopata – rangi, chenye damu, makamasi, chepesi,kigumu


NAMNA YA KUMCHUNGUZA AU KUMPAPASA:

- Mtoe mtoto nguo zote (pamoja na nepi) akiwa katika chumba chenye joto la wastani
o Mpime au chungunza kama ana homa – Joto la juu la mwili
o Angalia ngozi yake kama ana vipele, mchubuko au alama yeyote ambayo hakuwa nayo
o Angalia na kumpapasa kama ana uvimbe wowote(wa kujigonga au vinginevyo) au kidonda
o Angalia kama kuna kiungo kilichopinda isivyo kawaida (dalili ya kuvunjika au kuteguka)
o Chunguza tumbo lake kama limevimba isivyo kawaida, au kutoa sauti zaidi ya kawaida

Mfunike mtoto na kanga safi au kitambaa chochote chepesi kisafi kisha endelea kumchunguza
o Angalia masikioni kama kuna uchafu unaotoka kama usaha au damu
o Mpapase nyuma na mbele ya masikio kama kuna maumivu au uvimbe
o Angalia macho yake kama anaonyesha dalili ya umakini kwa anachokitazama au anazungusha macho isivyo kawaida
o Chunguza kama shingo imekaza/kukakamaa, au kukakamaa kwa kiungo kingine chochote.

N.B: Wakati wa kumchunguza mtoto usimuache aendele kulia, jaribu kufanya uchunguzi huu wakati unambembeleza na kumtuliza. Utafifi unaonyesha kumuacha mtoto alie sana bila kujaribu kumtuliza ina madhara katika ubongo wa mtoto unaokua.

Kama mtoto ananyonya waweza kuendelea kumnyonyesha wakati unatafuta sababu yake kulia. Kwa mtoto anayenyonya, akikataa kunyonya nakuendelea kulia tuu usimlazimishe, mpeleke hosipitali; mtoto anaweza kuwa na tatizo kubwa zaidi.

Kama umeshindwa kupata sababu yeyote au umepata sababu inayoashiria ugonjwa tafadhali muwahishe mtoto hosipitalini. Kulia sana huweza kuwa ndio dalili pekee ya mwanzo kwa mtoto inayoashiria malaria kali ya kupanda kichwani au homa ya uti wa mgongo, hivyo usipomuwahisha mtoto kwa matibabu madhara yanaweza kuwa makubwa zaidi.

Kama mtoto ana homa kali au mwenye maumivu makali kutokana na kuumia au kuvunjika unaweza kumpatia panado au dawa yeyote ya kushusha homa au kutuliza maumivu kisha mpeleke mtoto hosipitalini akafanyiwe uchunguzi zaidi na kutibiwa. Japo kushusha homa au kutuliza maumivu sio matibabu mbadala, haishauriwi kumuacha mtoto kukaa na homa muda mrefu au maumivu kwani inaweza kusababisha madhara mengine ya kiafya.


Kiungo kilichopinda isivyo kawaida

Kama umegundia kiungo kilichopinda isivyo kawaida (kama inavyoonekana kwenye picha) ikiashiria kuvunjika au kuteguka usijaribu kukirudisha kiungo hicho katika hali yake ya kawaida, unaweza kusababisha madhara zaidi. Kifungie kiungo hicho (mkono, mguu n.k) katika box au ubao bapa ili kuzuia mtikisiko kisha muwahishe mtoto hosipitalini.





Namna ya kuzuia mtikisiko
kipande cha box au kitu chochote kigumu

 Kwa mtoto aliyetoka kupata chanjo za sindano, maumivu yatokanayo na chanjo hii huweza kumfanya mtoto kulia sana na wakati mwingine kupata homa. Inashauriwa kumpa mtoto dawa ya kutuliza maumivu na homa kisha muangalie kwa masaa 24. Kama ukiona hali inazidi kuwa mbaya mpeleke hosipitalini. Pia Usimpeleke mtoto kwa chanjo akiwa na homa au akiwa katika matibabu ya ungojwa mwingine.

Monday, July 21, 2014

MAUMIVU YA KIFUA (CHEST PAIN)


 Kifua kuuma ni dalili ya magonjwa mengi sana, zaidi ya magonjwa 100 huweza kusababisha kifua kuuma.
 Lakini pia ni dalili ambayo haitakiwi kupuuzwa au kuchukuliwa kirahisi kwani inaweza kuwa dalili ya magonjwa hatari na yanayoweza kusababisha kupoteza maisha haraka – kama magonjwa ya moyo (heart attack) au ya mapafu (pulmonary embolism)
 Kutokana na umuhimu wa dalili hii, napenda tuangalie mambo machache ya muhimu kufahamu kuhusu maumivu ya kifua.

Angalizo: 

Usitumie ushauri na taarifa kutoka kwenye ukurasa huu kujichunguza au kujitibia mwenyewe nyumbani, Nenda kamuone daktari ili ufanyiwe uchunguzi sahihi na kutibiwa. Taarifa zilizoko kwenye ukurasa huu zikusaidie kutambua hatua za kuchukua upatapo na maumivu ya kifua au inapobidi kimsaidia mtu mwenye tatizo hilo.

MAGONJWA YASABABISHAYO KIFUA KUUMA NA DALILI ZAKE:

 

MAGONJWA YA MOYO:

 Mshituko wa moyo (Heart attack/ Angina Pectoris)
 Vijidudu kwenye moyo (infections) – (Pericarditis, myocarditis,endocarditis)
 Matatizo ya valve za moyo
 Magonjwa ya mshipa mkuu wa damu (aortic aneurysm, dissection)



Mshituko wa moyo(Heart Attack)
Dalili:
 Kifua kuuma kama mzigo mzito umekandamiza moyo
 Au maumivu makali kama mshale umekaa kwenye moyo
 Maumivu husikika upande wa kushoto wa kifua, sehemu ya katikati au yaweza kuwa popote kifuani
 Pia huweza kusikika kwenye bega, shingo, taya, mkono wa kushoto au hata kwenye meno (Radiating pain type).
 Kifua huwa kizito, na kujisikia kukosa hewa
 Moyo kuenda mbio
 Kutoka jasho jingi, kizunguzungu, kutapika au kwikwi isiyokatika
 Pia dalili nyingine huweza kujitokeza kama – kupoteza fahamu, tumbo kuuma n.k
 Maumivu huzidishwa na mishughuliko (activities/exertion) au msongo wa mawazo(stress). Kutulia au kupumzika (rest/relax) huleta nafuu au kuondoa maumivu.
 Homa hutokana na kuwepo kwa vijidudu (infection) kwenye moyo au damu.

MUHUMU: Ukipata dalili moja au zaidi kama zilizotajwa hapo juu, au maumivu ya kifua yasiyoisha zaidi ya dakika tano au yasiyotulia hata baada ya kupumzika au kutumia dawa za maumivu, tafadhali wahi hosipitali! Inapowezekana tafuta huduma ya matibabu ya haraka ya wagonjwa waliozidiwa(emergency care).




MAGONJWA YA KIFUA:

Damu kuvilia kwenye mapafu
(Pulmonary Embolism)
 Damu kuvilia kwenye mishipa ya damu ya mapafu (pulmonary embolism)
 Vijidudu kwenye mapafu – husababisha homa ya vichomi (Pneumonia, Bronchitis, Tuberculosis/TB,) n.k.
 Kujaa maji, damu au hewa kwenye mfuko wa nje wa mapafu (pneumothorax, haemothorax or pleura effusion)
 Saratani
Picha inayoonyesha damu iliyovilia kwenye mapafu (Pulmonary embolism)

Dalili:

 Haya husababisha maumivu ya kifua aina ya vichomi,
 Au maumivu makali wakati wa kupumua – kuvuta hewa
 Maumivu huwa popote katika kifua, bila kusikika nje ya kifua kama kwenye bega au shingo (non radiating type)
 Husababisha shida katika kupumua, mtu kujisikia kukosa hewa na kuhema haraka haraka
 Mara nyingine husababisha rangi ya midomo au mikono kubadilika kuwa blue(cyanosis)
 Homa au kutoka jasho sana hasa wakati wa usiku huashiria vijidudu – virusi, bacteria, TB nk.
 Mara nyingi huambatana na kikohozi – kikavu au chenye makohozi


MAGONJWA YA MFUMO WA CHAKULA:

 Kiungulia au Vidonda vya tumbo
 Michubuko au vijidudu kwenye njia ya chakula (oesophagitis)
 Magonjwa mengine ya njia ya chakula, tumbo, kongosho au hata ini.


Dalili:

 Husababisha maumivu ya kifua hasa sehemu ya chini, katikati ya matiti,
 Huweza kuwa kama moto, au maumivu tu makali katika eneo hilo
 Wakati mwingine husikika sehemu ya chini ya moyo upande wa kushoto
 Usambaaji wake(radiation) huelekea upande wa bega la kulia au mgongoni
 Mara nyingi huwa na uhusiano na chakula – maumivu wakati wa kumeza, baada ya kula, wakati mtu ana njaa, baada ya kula aina fulani ya vyakula, au akibadilisha utaratibu wa chakula.
 Kama tatizo limeshakuwa kubwa huweza kusababisha maumivu makali hata bila kuhusiana na chakula.

MAGONJWA YA NGOZI, MISULI NA MUFUPA YA KIFUA

 Moto wa mungu (Herpes zoster) kwenye eneo la kifua
 Magonjwa ya matiti
 Magonjwa ya mifupa au vishikizo vya uti wa mgongo
 Magonjwa ya mishipa ya fahamu ya kufua
 Michubuko, kuumia au kuvutika kwa misuli katika kifua
 Michubuko, vijidudu au kuumia mifupa, viungo(joints) au vishikizo vya viungo(tendons and ligaments) katika eneo la kifua
 Magonjwa mengine ya misuli na mifupa ya kifua

Dalili:

 Maumivu yanayosababishwa na magonjwa haya huweza kufana na maumivu yeyote yaliyotajwa hapo juu.
 Ni muhimu kujua historia au maelezo ya maumivu hayo kwa undani, kufanyiwa uchunguzi wa kina na vipimo pale vinapohitajika ili kujua tatizo.

MAGONJWA MENGINE NJE YA KIFUA YANAYOWEZA KUSABABISHA KIFUA KUUMA

 Magonjwa ya kisaikolojia au kuhema haraka karaka
 Sumu za aina fulani kama – lead, carbon monoxide
 Magonjwa ya Saratani


MUHIMU: 

Magonjwa yanayosababisha maumivu ya kifua, hasa yatokanayo na moyo au mapafu huweza kusababisha kupoteza maisha haraka sana kama yasipotibiwa kwa wakati. Tafadhali wahi hospitali ili upatiwe tiba mapema na kuokoa maisha yako. Usipuuzie maumivu ya kifua; Ni afadhali kumsumbua daktari kwa kuwahi hospitali na kukuta hakuna tatizo, kuliko kuogopa kumsumbua daktari halafu ukachelewa hospitali na kupata madhara ambayo yangeweza kuzuilika, au kupoteza maisha.

Sunday, June 15, 2014

KUTOKA JASHO JINGI (Exessive sweating or Diaphoresis)



Kutoka jasho (sweating) ni jambo la kawaida kiafya kwa binadamu. Kazi mojawapo ya ngozi ni pamoja na kutoa jasho – kitendo ambacho ni muhimu katika kuupooza mwili ili usitunze joto ndani zaidi ya inavyohitajika kiafya.

Vitengeneza jasho (sweat glands) vipo sehemu zote za mwili, ila mara nyingi zaidi jasho hutoka kwenye kwapa (under arm), kwenye nyayo (feet) au kwenye viganja vya mikono (palms), na hii hutosheleza kuupooza mwili. Kama hii haitoshelezi kupooza mwili basi jasho hutoka popote katika mwili.

Kutoka jasho jingi kwa ghafla (excessive sweating) sio kawaida, huenda ikawa ni dalili ya ugonjwa au tatizo katika mwili linalohitaji uchunguzi zaidi; au hali isiyokuwa ya kawaida katika mwili hata kama sio ugonjwa wenye kuhitaji matibabu.


SABABU ZA KUTOKA JASHO JINGI:

 

SABABU AMBAZO SIO UGONJWA  (Physiological causes)

• Mazoezi makali
• Hali ya hewa ya joto la juu kupita kiasi
• Vyakula vyenye viungo vikali: mfano pilipili kali
• Mabadiliko yatokanayo na kumaliza hedhi kwa wanawake (menopause)
• Kukumbuka jambo lililokuumiza sana (past trauma)
• Hisia kali (kama Hasira, uchungu, woga au wasiwasi)
• Maumivu makali – kama yatokanayo na kuvunjika, kuteguka kiungo kikubwa kama goti au bega
• Madawa ya kulevya – kama cocain, pombe kali; Pia kuacha ghafla au kukosa madawa haya kwa mtumiaji. Mara nyingi hii huambatana na hali ya kutetemeka-tetemeka (tremors)
• Aina fulani ya dawa za hosipitali – hasa za kutuliza maumivu au zile za matatizo ya kisaikolojia. Kuacha dawa hizi ghafla pia hupelekea kutoka jasho jingi kwa ghafla.
• Sababu za kurithi (genetical factors)


SABABU ZITOKANAZO NA UGONJWA  (Pathological causes)

• Homa kali (fever) – Jasho laweza kutoka kama dalili ya kuwa na homa, au baada ya kutumia dawa za kuondoa homa (kama panado) kama namna ya kuupooza mwili homa inapotoka.
• Vijidudi kwenye damu (infections)– Malaria, virusi (viral illnesses),bacteria n.k
• TB (Tuberculosis) – Jasho jingi hasa wakati mtu amelala, kupungua uzito na dalili nyingine.
• Magonjwa hatari ya moyo (heart attack, heart failure etc) – huenda yakaambatana na kifua kuuma, kukosa hewa, presha kushuka au moyo kwenda mbio.
• Magonjwa hatari ya mapafu – kama damu kuvilia kwenye mapafu (pulmonary embolism), maji kujaa kwenye mapafu(pulmonary oedema), hewa kuzunguka mapafu(pneumothorax)n.k – haya pia huambatana na dalili kama za magonjwa ya moyo zilizotajwa hapo juu.
• Sukari kushuka mwilini (hypoglycemia) – huenda ikaambatana na kuchanganyikiwa, kupoteza fahamu, au kuzimia ghafla. Huwapata sana wagonjwa wa kusukari, hasa wale wanaochoma sindano au kutumia aina fulani ya dawa za sukari.
• Madini joto kuzidi mwilini (hyperthyroidism) – kutoka jasho sana kwenye viganja vya mikono au nyayo wakati wote. Mara nyingi huambatana na dalili nyingine za ugonjwa huu.
• Hali ya presha kushuka sana (Shock) – Hii ni hali ya hatari na huhitaji matibabu ya haraka. Mgonjwa huwa wa baridi, aliyelegea na mwenye kutoka jasho jingi sana mwili wote.
• Kiarusi (stroke), au magonjwa mengine ya mfumo wa fahamu(nervous system) – haya pia huweza kusababisha jasho kutoka upande mmoja wa mwili hasa magonjwa ya uti wa mgongo
• Saratani za aina fulani – kama saratani ya damu (leukaemia)
• Sumu aina ya mercury na nyinginezo.

 Uonapo dalili kama zilizotajwa hapo juu ni muhimu kuwahi hosipitalini, kwani magonjwa mengi yanayosababisha jasho kutoka kwa wingi ni hatari na huweza kusababisha kupoteza maisha.
 Kama ni mgonjwa wa kisukari anza kwa kumpa kitu chenye sukari kama asali, sukari iliyokorogwa kwenye maji au soda. Kama hana fahamu weka kiasi kidogo chini ya ulimi, kisha mpeleke hosipitali.
 Mruhusu na kumsaidia mgonjwa kukaa kwa namna inayompa nafuu (comfortable position), usimlazimishe kulala au kukaa kwani magonjwa mengine huzidisha ukali/madhara kufuatana na namna ya ukaaji.
 Usimpe mtu anayetoka jasho jingi dawa ya usingizi kabla ya kujua sababu ya jasho kutoka.



JASHO KUTOA HARUFU MBAYA:

Jasho kutoa harufu mbaya sio ugonjwa ila ni hali inayomfanya mhusika kukosa raha na kumpa madhara kisaikolojia. Sababu zifuatazo hupelekea jasho kutoa harufu mbaya:
• Bakteria au fangasi waishio kwenye ngozi (normal skin flora)
• Aina ya vyakula vyenye harufu kali kama vile – vitunguu saumu (garlic)
• Madawa yenye harufu kali
• Magonjwa kama Ugonjwa wa figo ( uremia), Kisukari (DKA)
Kujua sababu inayopelekea harufu mbaya kutakuwezesha kujua njia bora ya kushughilikia tatizo hilo.


MADHARA YATOKANAYO NA KUTOKA JASHO KUPITA KIASI:

• Madini kuvurigika (electrolyte imbalance) – hii hutokana na kupotea kwa madini haya kwa njia ya jasho kama vile madini ya chumvi (Sodium)
• Kupungua maji mwilini (dehydtation) – Hutokea hasa katika mazingira yenye joto kali (kama Dar es salaam), na hii hupelekea mtu kujisikia kuchoka sana, kichwa kizito, kuumwa kichwa na kusikia kikaukiwa sana. Kunywa maji mengi (hasa yenye madini) na maji ya madafu huepusha tatizo hili
• Madhara ya kisaikologia – mtu anayetoka jasho sana kukosa raha, huweza kujiona sio wa kawaida na pengine kujitenga na wengine(isolation). Hali hii huweza kupelekea msongo wa mawazo (stress or depression)


MATIBABU:


Ni muhimu kutafuta sababu ya kutoka jasho jingi na kutibu chanzo hicho.
Kwa kuwa magonjwa mengi yanayoambatana na kutoka jasho jingi ni magonjwa ya hatari na yenye kuhitaji matibabu ya haraka, ni muhimu sana kutodharau hali ya kutoka jasho jingi ghafla. Muone daktari kwa ushauri, uchunguzi na inapobidi matibabu.

Kama hakuna magonjwa yanayohitaji matibabu, njia zifuatazo hutumika kutatua tatizo la kutoka jasho kwa wingi:
• Kuoga mara kwa mara – hii husaidia mwili kuwa katika hali ya kupoa hivyo kupunguza jasho, pia husaidia kupunguza vijidudu kwenye ngozi na harufu mbaya.
• Kupumnzika na kuwa katika hali ya utilivu (Relaxation) – Kusinga(massage), mazoezi ya kuvuta hewa nyingi(taking deep breaths) mazoezi ya yoga au kufanya mazoezi ya viungo mara kwa mara husaidia mwili kuwa tulivu (to relax) na hivyo kupunguza au kuondoa hali ya wasiwasi (enxiety) woga (fear) na msongo wa mawazo
• Dawa za kupaka – Zipo dawa za kupaka ambazo huzuia jasho lisitoke (antiperspirants) , na zipo ambazo husaidia kuondoa harufu mbaya (deodorants).
• Dawa za kumeza, Sindano na Matibabu ya upasuaji – huhitajika tu pale ambapo tatizo ni kubwa na linalomletea mhusika madhara ya kiafya au kisaikologia. Muone daktari wa magonjwa ya ngozi kwa ushauri zaidi.



Sunday, June 8, 2014

KWIKWI (Hiccups)

Kwikwi hutokana na kushtuka na kusinyaa kwa ghafla kwa misuli mikuu ya upumuaji (diaphragm) ambako hujirudia rudia na kusababisha hewa kuingia kwa kasi kwenye mapafu.

Hii husababisha milango ya sauti katika koo (vocal cords or voice making cords) kufunga ghafla na kutoa sauti inayosikika wakati wa kwikwi.

Kwikwi sio ugonjwa; kwikwi ya muda mfupi ni kero ndogo tu ambayo inapita, lakini kwikwi isiyokatika inaweza kuwa dalili ya tatizo lingine ambalo huenda likahitaji uchunguzi wa kitaalamu.

 

SABABU ZINAZOPELEKEA KUPATA KWIKWI;

• Kula haraka haraka au kula sana (kuvimbiwa)
• Kula vyakula vyenye viungo sana (very spicy foods)
• Kunywa vinywaji vyenye gesi(carbonated beverages) au vya baridi sana
• Ulevi au kunywa pombe nyingi kwa mpigo
• Upungufu wa maji na madini mwilini (dehydration)
• Tumbo kujaa gesi, asidi (hyperacidity) au vidonda vya tumbo

Sababu hizi mara nyingi husababisha kwikwi ya muda mfupi ambayo huisha bila kuhitaji matibabu wala uchunguzi wa kitaalamu.

SABABU NYINGINE (Rare but serious) ni pamoja na;

• Upungufu au kuvurigikwa kwa kiasi cha madini mwilini(electrolyte imbalances)
• Kukusanyika kwa sumu mwilini kama vile sumu ya figo (Uremia)
• Magonjwa ya mapafu kama vile vichomi(pneumonia), pumu(asthma), TB au maji kukusanyika nje ya mapafu(pleural effusion),
• Saratani au uvimbe kwenye mapafu, ubongo, uti wa mgongo au tumboni.
• Magonjwa ya moyo (heart attack, arrhythmias, infections to the heart)
• Kidole tumbo(Apendix illness) na magonjwa ya kufanania nayo
• Magonjwa ya Ini, kongosho au mfuko wa nyongo
• Madawa au kunywa sumu aina fulani
• Kuumia katika eneo la misuli ya upumuaji (diaphragm injuries).

Kwikwi itokanayo na matatizo haya huwa ya muda mrefu au inayojirudia rudia sana, na huisha tu kama tatizo lililosababisha likigundulika na kutibiwa. Ukiona dalili ya kwikwi isiyoisha tafadhali muone daktari.

  SABABU YA KISAIKOLOJIA (psychological reason)

Hii huwapata watu wachache. Watu hawa hujidhania kuwa wana kwikwi isiyokatika, hivyo huendelea kutoa sauti kama mtu mwenye kwikwi. Kwikwi ya aina hii haina mfumo maalum, na haitokani na kusinyaa kwa misuli ya upumuaji; kwa mtu mwenye tatizo hili ni muhimu kutafuta tatizo alilo nalo kisaikologia na kulitatua.

 

NAMNA YA KUZUIA KWIKWI

• Kula taratibu – haraka haraka hujaza gesi tumboni na kusababisha kuvimbiwa
• Kula kiasi kidogo kwa wakati – Inashauriwa kuongeza idadi ya milo kwa siku badala ya kiasi; milo mitano midogo midogo badala ya mitatu mikubwa kwa siku.
• Punguza au ondoa kabisa vyakula vyenye viungo vingi/vikali.
• Kunywa maji – Unywaji mzuri wa maji huzuia na kutibu kwikwi, pia hulinda mwili na maradhi kama vile upungufu wa maji na madini(dehydration) na figo kutofanya kazi vizuri.
• Fanya mazoezi - huboresha ufanyaji kazi wa mapafu na misuli ya upumuaji, pia husaidia kuongeza kinga mwilini na kuimarisha ufahamu (mind state)
Kuzuia kwikwi ni muhimu tu kwa wale wanaopata mara kwa mara.

 

MATIBABU YA KIENYEJI: (Usifanye kwa mtoto)

• Kumshitua mhusika, au kumzubaisha ili kuondoa mawazo yake kwenye kwikwi
• Kunywa glasi ya maji iliyojaa bila kukata pumzi
• Kubana pumzi na kuhesabu mpaka kumi
• Kuweka sukari chini ya ulimi
• Kulala. Usingizi ni dawa moja nzuri sana ya kwikwi
• Kwa mtoto anayenyonya waweza kumnyonyesha, au kumuweka begani acheue.
Kwiki ya kawaida huisha tu yenyewe bila kuhitaji tiba yeyote.

 

MATIBABU YA KITAALAMU

Muone daktari kwa matibabu kama
• Kwikwi haikatiki kwa muda mrefu (siku au zaidi),
• Kwikwi inakusababisha kuchoka sana,
• Kama mapigo ya moyo yanabadilika,
• Kama unashindwa kulala kutokana na kwikwi
• Kama inasababisha msongo mawazo kutokana na kujirudia mara kwa mara.

Kabla ya kuanzisha dawa ni muhimu kufanya vipimo ili kuhakikisha magonjwa yanayoweza kusababisha kwikwi yanapatiwa matibabu kama yapo.

Kama chanzo cha kwikwi kimefahamika katika uchunguzi, tibu chanzo na kwikwi itaisha.