Tezi Dume ni nini?
Tezi dume ni kiungo (organ) kimojawapo katika mfumo wa uzazi wa mwanaume.
Mwanaume huzaliwa na tezi dume yenye ukubwa sawa na punje ya ngano; kwa kadri anavyokua, tezi hii hukua hadi kufikia ukubwa wa sentimeta 4x2x3 (walnut size) katika umri wa utuuzima.
Ukuaji wa tezi hii kabla ya kubalehe huwa ni wa taratibu sana, ila katika kipindi cha kubalehe (puberty period) ukuwaji wake huwa wa haraka zaidi (sambamba na mabadiliko mengine katika mfumo wa uzazi wa mwanaume) hadi kufikia ukubwa uliotajwa hapo juu. Uzito wa kawaida wa tezi dume kwa mtu mzima hauzidi gram 25; huwa na ukuta mwororo (smooth surface) na ugumu wa wastani (firm texture).
Tezi dume ipo baada tu ya kibofu cha mkojo,imeuzunguka mrija wa mkojo unaotoka kwenye kibofu (urethra) na mbele ya sehemu ya mwisho ya utumbo mpana (rectum)
Kazi ya tezi dume
Tezi dume huzalisha maji maji ambayo yanasaidia kulinda mbegu za kiume wakati zinapopita katika mrija wa mkojo ili zisidhurike, na pia huzipatia mbegu hizo virutubisho (protection and nourishment of sperms)
Pia tezi dume inahusika katika kumfikisha mwanaume kileleni wakati wa tendo la ndoa; mwanaume huweza kufika kileleni kwa njia tu ya kuisinga (massaging) tezi dume kupitia njia ya choo (Anus)
Maradhi ya tezi dume:
Maradhi ya tezi dume yanaweza kugawanywa katika makundi makuu matatu:
1. Maambukizi ya tezi dume - Prostatitis
2. Kuvimba tezi dume - Benign prostate hyperplasia(BPH)
3. Saratani ya tezi dume - Prostate cancer
Maambukizi ya tezi dume:
Maambukizi ya tezi dume ( Prostatitis) yanaweza kutokana na vijidudu kama bacteria au wakati mwingine hujitokeza tu bila uwepo wa bacteria.
Asilimia 90 -95 ya maambukizi ya tezi dume ni yale yasiyotokana na vijidudu (non- bacterial prostatitis), husababisha maumivu ya muda mrefu ya uumeni (chronic pelvic pain syndrome) na hutibiwa na dawa mbalimbali zikiwemo za kupunguza uvimbe, maumivu, madhara ya kisaikologia na hata upasuaji.
Maambukizi yanayotokana na bacteria hutibiwa na dawa aina ya antibiotics.
Unashauriwa kumuona daktari kama una maumivu sehemu za uumeni, au kama unapata maumivu wakati wa kupata haja ndogo au kupitisha mbegu (ejaculation) wakati ufikapo kileleni, kwa uchunguzi zaidi.
Kuvimba tezi dume (BPH):
Kadri umri unavyosogea (kwa wanaume) ni kawaida kwa tezi dume kuendelea kukua kwa kiasi fulani. Asilimia 8 hadi 10 ya wanaume huwa na tezi dume iliyovimba katika umri wa miaka 35 hadi 40, na inakadiriwa hadi kufikia miaka 80 asilimia zaidi ya 80 ya wanaume huwa na tezi dume iliyovimba (BPH).
Tatizo kubwa litokanalo na kuvimba kwa tezi dume ni kuzuia haja ndogo (mkojo) usipite kwa urahisi, kubaki kwenye kibofu na wakati mwingine hupelekea figo kushidwa kufanya kazi vizuri na kufeli.
Dalili za kuvimba tezi dume ni pamoja na:
- Kukojoa mara kwa mara – kutokana na mkojo kutoisha kwenye kibofu (incomplete bladder emptying)
- Mkojo kutoka kwa kusita-sita (hesitance)
- Mkojo kutoka kwa udhaifu sana (weak stream)
- Mkojo kuja kwa kasi na ghafla na kusababisha kushindwa kuuzuia (urge incontinence)
- Mkojo kuendelea kidondoka kidogo kidogo baada ya kujisaidia (dribbling)
- Wakatu mwingine mkojo huweza kuziba ghafla na kusababisha maumivu makali.
- Pia inaweza kusababisha kujirudia –rudia kwa maambukizi ya mkojo(recurrent UTI)
Sio kila mwanaume mwenye tezi dume iliyovimba anayepata dalili hizi. Wapo ambao tezi dume ni kubwa sana lakini hawana dalili yeyote
Bado haijafahamika ni nini kinasababisha tezi dume kuvimba kupita kiasi kwa wanaume wengine na wengine haivimbi, pia haijulikani kwa nini wengine wanapata dalili wengine hawapati.
Saratani ya tezi dume:
Saratani ya tezi dume inaweza kumpata mwanaume yeyote, japo utokeaji wake kwa mwanaume chini ya miaka 50 ni wa nadra sana. Hii ni satarani ambayo hukua taratibu sana, na haionyeshi dalili yeyote wakati inapokuwa.
Umri mkubwa, kuwa mwafrika, historia ya saratani ya tezi dume au saratani ya matiti katika familia ni mambo ambayo yanaongeza uwezekano wa mtu kupata saratani hii. Pia vyakula vyenye mafuta sana, au mboga mboga chache vinakuweka katika hatari ya kupata saratani ya tezi dume.
Uchunguzi wa tezi dume.
Ukipata dalili kama zilizotajwa hapo juu, au hata bila dalili yeyote, ni vema kumuona mtaalamu kwa ajili ya uchunguzi wa tezi dume. Uchunguzi wa mara kwa mara unataweza kugundua tatizo hata la saratani kabla haijasambaa na kukuwezesha kupata matibabu ya kuhakika.
Mtaalamu wa afya atafanya moja kati ya haya, au anawaza kufanya yote matatu kulingana na atakavyoliona tatizo lako:
1. Uchunguzi kupitia njia ya choo: (Digital rectal examination) – Ataweza kuchunguza ukubwa (size), ugumu (texture) na wororo (smoothness) wa tezi dume. Njia hii inaweza kutofautisha saratani na BPH japo sio njia ya uhakika sana kuzitofautisha. Wakati mwingine saratani inaweza kufana na BPH katika kipimo hiki.
2. Kipimo cha damu: Mtaalamu anaweza kuamua kuchukua kipimo cha damu kuchunguza aina ya chemikali inayozalishwa na tezi dume (Prostate specific antigen – PSA). Hii pia sio njia sahihi sana kutofautisha saratani na BPH. PSA inaweza kupanda kutokana na BPH, maambukizi ya tezi dume au hata baada ya kuingiziwa mpira wa mkojo. Hivyo majibu ya PSA yakiwa juu uchunguzi zaidi utahitajika. Kama PSA iko kawaida uwezekano ni kwamba tatizo haliko kwenye tezi dume!
3. Kipimo cha mkojo: Mtaalamu anaweza kukushauri kupima mkojo ili kuchunguza maambukizi kwenye mkojo au tezi dume.
Matibabu:
1. Maambukizi ya tezi dume hutibiwa na antibiotics (kama yamesababishwa na bacteria) na dawa za kupunguza maumivu na kuvimba (inflammation).
2. Matibabu BPH yanaweza kuwa dawa au upasuaji
o Dawa ziko za aina mbili – aina ya kwanza itasaidia misuli ya kibofu cha mkojo kulegea na hivyo kupunguza dalili zitokanazo na kuvimba tezidume. (Alpha blockers)
o Aina ya pili husaidia tezi dume isiendelee kukua na wakati mwingine (sio wakati wote) huisababisha kusinyaa (Alpha-reductase inhibitors)
o Kwa tezi dume ambazo hazisababishi dalili zozote madaktari wengi hupenda kufanya uangalizi wa kaaribu bila matibabu yeyote (watchful wait).
o Kwa wale walioanza dawa, mara nyingi huhitaji kutumia dawa hizo maisha yao yote au mpaka upasuaji utakapofanyika
o Upasuaji unaweza kufanyika kupitia njia ya mkojo, au kupitia tumboni chini ya kitovu.
3. Matibabu ya saratani ya tezi dume yanategemea na kiasi cha usambaaji wa saratani hiyo.