Watoto walio chini ya miaka miwili hutumia kulia kama lugha yao kuu kuwasilisha mahitaji yao kuliko lugha nyinginezo. Ni muhimu kwa wazazi kumuelewa mtoto wao ili waweze kujua wakati analia kawaida, na wakati analia zaidi ya kwawaida. Pia ni vyema kumjengea mtoto tabia ya kutumia lugha nyingine tofauti na kulia kadri anavyokua.
Ni mara chache sana kwa mtoto aliye chini ya miaka miwili kulia sana bila sababu, hivyo haishauriwi kupuuzia tu au kuendelea kumbembeleza bila kujua sababu inayomfanya alie; ni vyema kuchunguza kwanza sababu inayomfanya aendelee kulia.
Kwa upande mwingine wazazi wengi, hasa wale wapya, huhamaki wanapoona mtoto analia kuliko kawaida na kushindwa kujua wafanye nini kumsaidia. Ukurasa huu ukusaidie kama mzazi au mlezi wa mtoto kufahamu hatua za kuchukua unapokuwa na mtoto wakati analia sana.
SABABU ZA MTOTO KULIA SANA
- Homa ya uti wa mgongo- Malaria kali (ya kichwa)
- Homa ya masikio
- Kuumia au kuvunjika
- Tumbo kuuma au gesi tumboni
- Michubuko au vidonda mdomoni, kooni au vitokanavyo na nepi
- Choo kigumu (constipation)
- Kuchoka sana au kushindwa kulala
- Njaa ya muda mrefu
- Kuumwa na mdudu kama siafu n.k.
- Nguo kubana au kufunikwa sana
- Kutaka kuwa na mzazi wake!
- Magonjwa ya kisaikolojia
UFANYE NINI MTOTO AKIWA ANALIA SANA:
•NAMNA YA KUM'BEBA:
- Mbebe mtoto katika hali itakayompa utulivuo Mweke begani au kumpakata kama inavyoonekana kwenye picha.


o Hali ya utulivu humwezesha mtoto aliyechoka sana kupata usingizi.
o Kumweka begani husaidia kuondoa gesi tumboni.
• NAMNA YA KUMBEMBELEZA
- Haishauriwi kumrusha rusha mtoto au kumtingisha kwa nguvuo Huongeza maumivu kwa mtoto aliyeumia au kuvunjika
o Humfanya mtoto mwenye homa au tatizo la tumbo kujisikia vibaya zaidi
o Humfanya mtoto aliyechoka sana kushindwa kulala na kumfanya azidi kulia.
• MAMBO YA MUHIMU KUCHUNGUZA:
- Muda na mazingira alipoanza kulia:o Hali ya mtoto kabla hajaanza kulia – aliyelala, anacheza, anakula, n.k
o Kilichotokea au kusababisha akaanza kulia – kushtuka, kuanguka, kula, ghafla tu n.k
o Mazingira aliyokuwepo alipoanza kulia – chumbani, bafuni, kwenye majani, jikoni n.k
Chakula :
o Muda aliokula mlo wa mwishoo Chakula alichokula na kiasi alichokula.
o Mabadiliko katika chakula chake (hata kama ni madogo) – uandaaji au kumlisha
o Kwa mtoto anayenyonya mama achunguze kama kuna mabadiliko yeyote katika maziwa yake (kama maziwa hayatoki, au yanauma au chuchu zina michubuko)
Choo chake:
o Muda alipopata choo mara ya mwisho (kikubwa au kidogo)o Muda aliobadilishwa nepi; Pia chunguza nepi aliyovaa.
o Muonekano wa choo alichopata – rangi, chenye damu, makamasi, chepesi,kigumu
• NAMNA YA KUMCHUNGUZA AU KUMPAPASA:
- Mtoe mtoto nguo zote (pamoja na nepi) akiwa katika chumba chenye joto la wastanio Mpime au chungunza kama ana homa – Joto la juu la mwili
o Angalia ngozi yake kama ana vipele, mchubuko au alama yeyote ambayo hakuwa nayo
o Angalia na kumpapasa kama ana uvimbe wowote(wa kujigonga au vinginevyo) au kidonda
o Angalia kama kuna kiungo kilichopinda isivyo kawaida (dalili ya kuvunjika au kuteguka)
o Chunguza tumbo lake kama limevimba isivyo kawaida, au kutoa sauti zaidi ya kawaida
Mfunike mtoto na kanga safi au kitambaa chochote chepesi kisafi kisha endelea kumchunguza
o Angalia masikioni kama kuna uchafu unaotoka kama usaha au damu
o Mpapase nyuma na mbele ya masikio kama kuna maumivu au uvimbe
o Angalia macho yake kama anaonyesha dalili ya umakini kwa anachokitazama au anazungusha macho isivyo kawaida
o Chunguza kama shingo imekaza/kukakamaa, au kukakamaa kwa kiungo kingine chochote.
N.B: Wakati wa kumchunguza mtoto usimuache aendele kulia, jaribu kufanya uchunguzi huu wakati unambembeleza na kumtuliza. Utafifi unaonyesha kumuacha mtoto alie sana bila kujaribu kumtuliza ina madhara katika ubongo wa mtoto unaokua.
Kama mtoto ananyonya waweza kuendelea kumnyonyesha wakati unatafuta sababu yake kulia. Kwa mtoto anayenyonya, akikataa kunyonya nakuendelea kulia tuu usimlazimishe, mpeleke hosipitali; mtoto anaweza kuwa na tatizo kubwa zaidi.
Kama umeshindwa kupata sababu yeyote au umepata sababu inayoashiria ugonjwa tafadhali muwahishe mtoto hosipitalini. Kulia sana huweza kuwa ndio dalili pekee ya mwanzo kwa mtoto inayoashiria malaria kali ya kupanda kichwani au homa ya uti wa mgongo, hivyo usipomuwahisha mtoto kwa matibabu madhara yanaweza kuwa makubwa zaidi.
Kama mtoto ana homa kali au mwenye maumivu makali kutokana na kuumia au kuvunjika unaweza kumpatia panado au dawa yeyote ya kushusha homa au kutuliza maumivu kisha mpeleke mtoto hosipitalini akafanyiwe uchunguzi zaidi na kutibiwa. Japo kushusha homa au kutuliza maumivu sio matibabu mbadala, haishauriwi kumuacha mtoto kukaa na homa muda mrefu au maumivu kwani inaweza kusababisha madhara mengine ya kiafya.
![]() |
| Kiungo kilichopinda isivyo kawaida |
Kama umegundia kiungo kilichopinda isivyo kawaida (kama inavyoonekana kwenye picha) ikiashiria kuvunjika au kuteguka usijaribu kukirudisha kiungo hicho katika hali yake ya kawaida, unaweza kusababisha madhara zaidi. Kifungie kiungo hicho (mkono, mguu n.k) katika box au ubao bapa ili kuzuia mtikisiko kisha muwahishe mtoto hosipitalini.
![]() |
| Namna ya kuzuia mtikisiko |
![]() |
| kipande cha box au kitu chochote kigumu |
Kwa mtoto aliyetoka kupata chanjo za sindano, maumivu yatokanayo na chanjo hii huweza kumfanya mtoto kulia sana na wakati mwingine kupata homa. Inashauriwa kumpa mtoto dawa ya kutuliza maumivu na homa kisha muangalie kwa masaa 24. Kama ukiona hali inazidi kuwa mbaya mpeleke hosipitalini. Pia Usimpeleke mtoto kwa chanjo akiwa na homa au akiwa katika matibabu ya ungojwa mwingine.




Vizuri nimejifunza vingi mno
ReplyDeleteNimekupata vema
ReplyDeleteMtoto wangu anapoanza kulia akinyonyeshwa hutulia lakini akiacha tu kunyonya anaanza kulia,tulienda hospital docter alisema mtoto huenda hunyonyweshi kwa muda mrefu na huenda hanyoshweshi kwa namna nzuri ambayo hupelekea gesi kujaa tumbuni na kusababisha maumivu makali ya tumbo.Hivyo ushauri wa docter umefuatwa lakini bado mtoto analia sana namba ushauri wenu wandugu
ReplyDeleteJaribu kuona kama ni gesi mcheurishe
DeleteAsante kwa ushauri ila mimi nauliza,nini kifanyike kwa mtoto anayelia sana kwa sababu ya kutaka kuwa na mzazi wake na haiwezekani kwa wakati huo?
ReplyDeleteAsante