Saturday, December 3, 2016

ULIYAJUA HAYA KUHUSU VIRUSI VYA UKIMWI (VVU)?






VVU DUNIANI
**Afrika chini ya jangwa la Sahara tunabeba asilimia zaidi ya 70 (70%) ya maambukizi ya ukimwi wote duniani!!

**Idadi ya virusi mwilini ikiwa pungufu kabisa (undetectable) kutokana na matumizi mazuri ya dawa unaweza kuishi maisha ya kawaida kabisa bila kusababisha maambukizi mapya kwa uayeshirikiana nae! 
 
**Inawezekana kabisa kupata watoto wasio na vvu, pia kuishi na mtu asiye na vvu bila kumuambukiza!!


 *     Dalili ya mwanzo kabisa ya kuwa umepata maambukizi ya VVU ni homa ya koo – kama mafua tu!

*     Mtu mwenye maambukizi mapya ya VVU ni rahisi zaidi kumuambukiza mtu mwingine (mara 26 zaidi katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo) kuliko yule mwenye maambukizi ya muda mrefu!

*     Siku 30 za mwanzo baada tu ya mtu kupata maambukizi ya VVU ndio siku ambazo ni rahisi zaidi kumuambukiza mtu mwingine kuliko kipindi kingine chochote cha ugonjwa huu!

*     Asilimia 30 hadi 50 (30%-50%) ya maambukizi mapya hutokea katika siku 30 za mwanzo za ugonjwa huu!

*     Maambukizi ndani ya wanandoa ni zaidi ya asilimia 55 hapa nchini (Tanzania) utafiti umeonyesha! Kuwa katika ndoa ni moja ya vihatarishi vya kupata maambukizi ya VVU kutokana na kasi kubwa ya kukosekana kwa uaminifu katika ndoa! (ulisema utafiti huo)

*     Kipimo cha VVU tunachotumia katika uchunguzi hapa nchini hugundua maambukizi baada ya miezi mitatu au zaidi wakati mwili ukishatengeneza kinga ya kupambana na VVU; hivyo watu wengi hawajitambui kama wana maambukizi mapya ya VVU!

*     Vipo vipimo vinavyoweza kugundua maambukizi hata baada ya siku tatu tangu kuathirika; vipimo hivi hutumika katika mazingira maalumu tu kwa sasa, havijidhinishwa bado kutumika kwa kila anayepima au aliye hatarini!

*     Maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwanda kwa mtoto hutokea mtoto akiwa tumboni (5%), wakati wa kuzaliwa (45%) na wakati wa kunyonyesha (40%).

*     Upimaji wa VVU wakati wa ujauzito na matumizi sahihi ya dawa za kuongeza kinga (ART) kumepunguza maambukizi haya hadi asilimia chini ya 5 (<5%)!

NINI UFANYE:


*     Ijue afya yako – Ni muhimu sana kujitambua kama una maambukizi ya VVU au la. Kufahamu hali ya afya yako kutakuwezesha wewe kujikinga au kuwakinga wengine ambao hawajapata maambukizi pia!

*     Kuwa Mwaminifu – Kwa Mungu, kwako wewe mwenyewe na kwa mpenzi wako mmoja! Uaminifu ndio jambo la kwanza kabisa litakalokuhakikishia kutopata maambukizi mapya au kumpelekea mwingine maambukizi mapya!

*     Pata ushauri – Ni muhimu sana kujifunza njia mbalimbali za kujikinga usipate maambukizi ya VVU. Unaweza kujikinga wewe mwenyewe, unaweza kumkinga mwenzi wako, pia unaweza kuwakinga watoto wako kabla na baada ya kuzaliwa!

*     Tumia dawa kwa usahihi – Ikiwa umepata maambukizi ya VVU ni muhimu sana kutumia dawa za kuongeza kinga kwa uaminifu na usahihi kabisa! Washauri wa afya watakupa mafunzo haya!

MATUMIZI YA DAWA ZA KUONGEZA KINGA (ART)


Tiba kwa kila muathirika


*     Sheria mpya ya matumizi ya dawa za VVU inamtaka kila anayepima na kugundulika na maambukizi ya VVU kuanza kutumia dawa bila kujali wingi wa kinga yake.

*     Hii inasaidia kuzuia VVU wasiendelee kumshambulia muathirika, husaidia kinga isipungue mwilini, huzuia magonjwa nyemelezi yasimpate aliyeathirika, lakini pia hupunguza sana idadi ya VVU mwilini hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa muathirika kumuambukiza mwingine VVU (Mwenzi au mtoto)!

Tiba kama kinga


*     Dawa za VVU hutumika pia kama kinga kuzuia maambukizi mapya (Post-exposure prophylaxis).

*     Itokeapo mmoja ambaye hajaathirika amejikuta katika hali hatarishi (kubakwa, kushirikiana na mtu aliyeathirika bila kinga, kujichoma na sindano iliyomchoma aliyeathirika, au mtoto aliyezaliwa kwa mama aliyeathirika) hupewa dawa hizi kama kinga ya maambukizi mapya ndani ya masaa 72.

*     Pia dawa za VVU huweza kutumika kama kinga kabla ya tendo la ndoa kwa wale wenye mahusiano ambao mmoja ni muathirika na mwingine sio muathirika wanapohitaji kushiriki tendo bila kinga! (Pre-exposure prophylaxis) (Hii haijawa rasmi katika nchi yetu kwa sasa).

NENO LA MWISHO:


*     Kuathirika na vvu sio mwisho, maisha yanaendelea. Ijue afya yako! Nenda kapime! Tumia dawa kwa uaminifu na usahihi siku zote! Kwa kufanya hivi utawakinga uwapendao! Japo tiba kamili haijapatikana iliyothibitishwa kutibu VVU na utafiti unaendelea, tiba zilizopo kwa sasa zinaweza kukupa maisha ya kawaida kabisa!  Kuacha dawa ni hatari sana kwani vvu hurudi kwa kasi na kwa ukali zaidi, na mara nyingi huwa sugu kwa dawa! Hata kama vvu wako chini kabisa na kinga yako ni nzuri kabisa usiache dawa!

No comments:

Post a Comment